Tuesday, June 14, 2016

MPENZI WANGU WA ENZI


Jioni usikawie
Moyo umejawa hamu
Mashaka usinitie
Maumivu ni haramu
Usinifanye nilie
Nikameza hata sumu
Fika nami nitulie
Zirudi zangu fahamu
Haki yangu nipatie
Nijihisi mwanadamu
Mlete nimsikie
Anene yake matamu
Nimeshampenda Mie
Mimi naye damudamu
Mpenzi wangu wa enzi, asilani sitomwacha.

Moyo unataka tiba
Mlete kwangu haraka
Kinada akipuliza
Roho inaliwazika
Akinena kwa mahaba
Huzidi yangu faraja
Shaka yote huniisha
Akiwa nami faragha
Napenda anapocheka
Anapenda nikideka
Jioni naomba fika
Kabla hamu haijanisha
Mpenzi wangu wa enzi, asilani sitomwacha.

Jua nenda pumzika
Muda umeshawadia
Sitaki kufedheheka
Wasiwasi kunitia
Nafsi haitoridhika
Machoni nisipomtia
Karibu ninamtaka
Kutwa namsubiria
Hapa ataliwazika
Kwa wake mahabubia
Hanjumati nitapika
Nyimbo nitamuimbia
Mimi kwake nishafika
Na kwangu keshatulia
Mpenzi wangu wa enzi, asilani sitomwacha.

(c) Zuhura Seng'enge
     ~ A. L 2016

https://s-media-cache-ak0.pinimg.com/236x/9a/25/0f/9a250f4c2f284631c0d2ea11a58139c9.jpg

3 comments:

Please share your thoughts and feelings..