Showing posts with label maisha. Show all posts
Showing posts with label maisha. Show all posts

Friday, January 2, 2015

Tufurahi.

TUFURAHI.
Umebadili maisha yangu,
Ukauteka na moyo wangu,
Mapenzi yako asali yangu,
Amani na furaha ni nyingi ukiwa kwangu.


Uzima wako faraja yangu,
Ucheshi wako liwazo langu,
Ukweli wako heshima yangu,
Nitunze nikutunze daima ukae kwangu.

Tusisikilize yale ya watu,
Kuaminiana jukumu letu,
Kusalitiana tusithubutu,
Tufurahi kila siku upendo ukae kwetu.


Tuwe kitu moja tupange yetu,
Tukishikamana ushindi wetu,
Tukivumilia mavuno yetu,
Tumuombe nae Mungu mazuri yapite kwetu.

©Zuhura Seng'enge
    01/10/2014.

(Please share, leave a comment)

Thursday, December 4, 2014

YA DUNIA.

Nimechoka kuvumilia, maudhi haya,
Nimechoka kusikia, wanawake wakilia,
Kila kona ya dunia, watoto wanaumia,
Nimechoka kupokea, 
Lawama na vitisho,
Kila ninapoangalia, ni mauaji ya albino,
Watu wanateketea;
Ubakaji, ukeketaji, unyanyasaji wa jinsia,
Utu umeshapotea.

Rushwa nayo yachochea, watu kesi kuzushiwa,
Vijana, wazee, madawa kuyatumia,
Afya zao kujihatarishia,
Bidhaa za bei chee, ndizo tunang'ang'ania,
Nyingi feki twasikia, bado tunakazania? 
Iko wapi ile nia, ya maisha kujijengea? 
Tumezongwa na dunia;
Wadada kusaka pesa, wakaka kuuza sura
Viwanja kujitanua, elimu kuipu'za.

Nao wenye nyingi ndoto, kazi hawashikilii
Hawaachi kupiga zogo, wakazisaka rupia,
Wanazidi likosa soko, maisha kuyajutia
Mengi nayafikiria, yaumiza watanzania,
Nimechoka kuvumilia, maudhi nazo ghasia,
Haki naitamania, amani ninaililia,
Wazazi nipeni elimu, niyashinde ya dunia
Wazazi nipeni elimu, isinishinde dunia.

Zuhura Seng'enge.
02/10/2014.
(Please share, leave a comment)

KWAKO NINATAMANIA.

Asubuhi inapofika maswali mengi hunijia
Wapi nitakwenda?
Nini nitakula?

Nikitangatanga kiguu na njia
Jua nalo likianza kusogea
Najiuliza wapi nitaanzia
Mawazo yanivaa na kutonesha vidonda

Maisha ya zamani nayatamania
Niliishi kwa amani sikuwahi fikiria
Kama shilingi mia itakua adimu,
Kama mkate ulooza nitalilia.

Usiku unapoingia hofu nyingi hunikaribia
Nani atanidhuru?
Wapi nitajilaza?

Ninaangaza huku na huko
Kutafuta hata boksi na mfuko
Tumbo likiunguruma kwa njaa
Ni siku ya tatu sasa, naanza kukata tamaa

Mvua ikininyeshea nimekaa pweke nikilia
Miaka sita nipo kitaa ndoto zangu zinanikimbia.

Asubuhi inafikia na huzuni yanivamia
Safari nyingine kiguu na njia
Kutafuta pakufikia

Nikigonga kwako nipokee
Hata shilingia mia nitolee
Nipate maji na andazi
Nisijechetuka nikafa jambazi.

Ewe unayetupa chakula
Huogopi hata Mungu?
Wengi tunakililia
Tulikombe hata jungu.

Usione udhia.

Zuhura Seng'enge.
20/11/2014.

(Please share, leave a comment)