Thursday, December 25, 2014

KAMA KIJANA HURU.

Kama kijana huru ninashukuru
Mungu kwa kuzaliwa kipindi uhuru umeshaingia
Kwa kulikuta taifa limeshazaliwa
Kwa kuikuta amani imeshajengeka
Kama kijana huru ninashukuru
Mashujaa walioipigania na kutetea uhuru
Viongozi, wanajeshi na wananchi waliojitoa kila siku
Wakayaona mauti na bado wakazidi kuchonga mikuki
Wakapigwa mijeledi na bado wakashika bunduki
Kama kijana huru ninashukuru
Waliotangulia kabla yetu kwa jasho na damu
Walilomwaga kukataa ukoloni wakavikwa utumwa
Wakashuhudia watoto wao wakivuliwa utu na kupigwa mitama
Kama kijana huru ninashukuru
Mungu kuzaliwa kipindi cha uhuru.

Kama kijana huru ninajukumu
La kuthamini utu na maisha ya mtanzania mwenzangu
La kuendeleza hekima na busara za waliopita kabla yangu
Waliojua maana ya uzalendo na
Wakajenga nchi kwa vitendo
Kama kijana huru ninajukumu
La kutetea haki za msingi za mtanzania mwenzangu
La kuhakikisha demokrasia ya maneno inaangamizwa kwa nguvu
Na vijana wa kitanzania wanaacha uvivu
Kama kijana huru ninajukumu
La kupambana na maadui wa maendeleo ya mtanzania
Ikiwemo ufisadi, rushwa, ubaguzi na imani za kishirikina
La kuelimisha jamii na kuifungua macho
Kua maana ya kua huru ni kuthamini na kuendeleza kidogo ulichonacho
Kua ujinga na kupuuzia uovu ndio chanzo cha machafuko
Kama kijana huru ninajukumu
La kuendeleza amani, upendo na uhuru.

Kama kijana huru ninahaki
Ya kujua ukweli na sio kuwekwa gizani
Ya kupata vizuri bila kupimwa mizani
Ya kupinga uonevu hasa kwa wanyonge na masikini
Ya kudai uhuru wangu, na mchango wangu kuuthamini
Kama kijana huru ninahaki
Ya kutimiziwa haki zangu za msingi;
Elimu bora, afya bora, usalama wa maisha na mali
Ila yasikitisha kuona zinazidi kudorora hali
Huduma mbovu, mishahara midogo na elimu ya dafutari
Kama kijana huru ninahaki
Ya kujua miaka 53 ya uhuruImenipa nini
Na kutambua kwa miaka 53Ninajivunia kitu gani.

©Zuhura Seng'enge 
  09/12/2014.

(Please share, leave a comment)

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..