Monday, December 8, 2014

UNAFURAHIA KUA MTANZANIA HURU?

Tanganyika huru,

Ndilo lilikua lengo kuu la baba wa taifa

Tanganyika shujaa,

Ndio uliokua msimamo mkuu wa baba wa taifa

Tanganyika endelevu,

Ndio iliokua jitihada kuu ya baba wa taifa

Na ujinga, maradhi, umasikini

Ndio yaliyokuamapambano makuu ya baba wa taifa.

Ni miaka 53 tangu uhuru utangazwe Tanganyika
Mwalimu alijitoa kuhakikisha tunasonga mbele watanganyika
Katika kipindi cha uhai wake alisisitiza sana juu ya upendo na umoja
Akijua Ipo siku yeye na sisi hatutokua tena pamoja
Tukaapa kuyafuata mafundisho aliyotuasa
Tukaahidi kutekeleza maagizo aliyoyaacha
Kwa machozi tena ya kwikwi, tukimkufuru hadi na Mungu

Tukatoa vyetu viapo, 'Tanganyika shujaa, Tanganyika huru'

Na tukasema kwa kishindo, 'Mtanganyika kabla ya mzungu'

Wanafiki!!

Tulijipamba kwa tabia nzuri mbele ya macho ya watu
Tukafuata kama kondoo wema kumbe asili yetu ni chatu
Ahadi nyingi tukazitoa na mipango lukuki lukuki
Watanzania bila kujua wakaukumbatia mkuki
Tukawa sababu ya taabu na dhiki
Tukajenga kati yetu chuki
Ujinga, maradhi, umasikini, vikatawala jamii zetu
Na sasa vimezaa watoto, wanaotawala maisha yetu;
Siasa chafu, ufisadi, rushwa, ujambazi, uvivu, unyanyasaji
Udini na ukabila, imani za kishirikina, ukatili na mauaji
Ndizo zimekua wimbo wa taifa
Nasi tumekaa tukitazama watoto wetu wakiangamia
Maradhi haya yakijenga donda ndugu katika nafisi zetu
Katika maisha yetu.

Tanzania huru, Tanzania shujaa, Tanzania endelevu
Lengo la mwalimu
Leo miaka 53 maadhimisho ya siku yetu
Tunajivunia kitu gani katika kua huru?
Zaidi ya kuongeza na kudai ushuru
Zaidi ya kutia giza kwenye nuru
Maendeleo? Ndio yapo kadhaa
Je yana thamani gani kama bado tunakufa na njaa?
Je yana thamani gani kama utu, upendo, umoja na ukweli ndio yetu karaha?

Tafakari, chukua hatua.
Hongera kwa kuiona miaka 53 ya uhuru Tanzania bara.

©Zuhura Seng'enge.
  09/12/2014.

(Please share, leave a comment)

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..