Thursday, June 16, 2016

Watoto Ndiyo Taifa



Natamani kuwa na jamii yenye amani
Niione machoni
Isiishie ndotoni,
Jamii ambayo watoto wana furaha
Wakiimba na kucheza
Hadithi kusimuliana,
Mahali watakapopendwa na wazee na vijana
Mahali watakapokuwa salama,

Jitihada za maisha bora ziwe kwa watoto
Wapate urithi kwa kzazi kijacho.

Natamani kuwa na jamii watakayopendwa watoto
Isiyotumia maumivu yao
Kuzichuma mali,
Natamani kuona wakipata haki zao
Mahali tabasamu lao
Litathaminiwa kuliko dhahabu,
Wasipotumikishwa wala kufanywa kama bidhaa
Wasipotelekezwa wakaja kufa kwa njaa
Wakiwa pweke kwenye dunia,
Natamani jamii itakayo wajali
Ikawaweka mbali na vitendo vya ukatili.

Natamani kuwa na jamii watakayothaminiwa watoto
Mahali Sauti zao
Zitasikiwa na wote,
Elimu yao kupewa kipaumbele
Mahali wasipolazimishwa
Kuuvunja undugu,
Na akili zao kutopotoshwa kwa uongo
Chuki ikajaa mioyoni mwao
Wakasahau kuwa na upendo,
Natama jamii ambayo watoto wataishi bila woga
Mahali salama penye tumaini na faraja.

Watoto ni baraka kwenye maisha,
Watoto ndiyo nuru kwenye kiza,
Watoto ni tumaini, watoto ni zawadi
Watoto ndiyo taifa.

*Translated From English

(c) Zuhura Seng'enge
        ~ A. L 2016
www.Zuhurasaad22.blog spot.com



Tuesday, June 14, 2016

MPENZI WANGU WA ENZI


Jioni usikawie
Moyo umejawa hamu
Mashaka usinitie
Maumivu ni haramu
Usinifanye nilie
Nikameza hata sumu
Fika nami nitulie
Zirudi zangu fahamu
Haki yangu nipatie
Nijihisi mwanadamu
Mlete nimsikie
Anene yake matamu
Nimeshampenda Mie
Mimi naye damudamu
Mpenzi wangu wa enzi, asilani sitomwacha.

Moyo unataka tiba
Mlete kwangu haraka
Kinada akipuliza
Roho inaliwazika
Akinena kwa mahaba
Huzidi yangu faraja
Shaka yote huniisha
Akiwa nami faragha
Napenda anapocheka
Anapenda nikideka
Jioni naomba fika
Kabla hamu haijanisha
Mpenzi wangu wa enzi, asilani sitomwacha.

Jua nenda pumzika
Muda umeshawadia
Sitaki kufedheheka
Wasiwasi kunitia
Nafsi haitoridhika
Machoni nisipomtia
Karibu ninamtaka
Kutwa namsubiria
Hapa ataliwazika
Kwa wake mahabubia
Hanjumati nitapika
Nyimbo nitamuimbia
Mimi kwake nishafika
Na kwangu keshatulia
Mpenzi wangu wa enzi, asilani sitomwacha.

(c) Zuhura Seng'enge
     ~ A. L 2016

https://s-media-cache-ak0.pinimg.com/236x/9a/25/0f/9a250f4c2f284631c0d2ea11a58139c9.jpg