Wednesday, December 20, 2017

SEMA NAMISema nami mwenzio
Ukimya sio rafiki wanimaliza moyo
Sema nami kwa vituo
Ukishusha pandisha pumzi mate yateremke taratibu kwenye koo
Sema nami kwa upole
Kama anavyosemezwa mtoto
Usininyooshee kidole
Nishike nibembeleze kidogo
Sema nami ukicheka
Macho yakitabasamu
Kama kiziwanda nikideka
Ndivyo maongezi yawa matamu
Sema nami nijaze hamu
Ya kubonga nawe kila siku
Wengine waombe zamu
Iwakamate shauku
Sema nami kwa ile sauti
Ile inayonipa njozi
Wakinikuta mahututi
Ujue sababu ni hayo mapozi
Chemchem ya furaha inapofurika
Hadi yanitoka machozi
Sema nami uwe mkombozi
Wa huzuni na majonzi yangu
Sema nami jaka moyo
Lisikumbatie nafsi yangu
Sema nami kwa vituko
Nicheke nipate afya
Mwili uingiwe muamko
Nikohoe, nikipige chafya
Sema we sio kibogoyo
Maneno waweza unda
Usiwe na choyo
Sikio lataka lake tunda
Sema nami kwa hisia
Nizame kama majini
Sema nami nije hadithia
Uniwekavyo makini.

Sema nami tuyamalize
Yanayotutia ukimya
Haraka tuteketeze
Amani yanayotunyima
Sema nami tuyajenge
Penzi lipate sitawi
Tusijeingia mkenge
Mapungufu kuyaita uchawi
Sema nami usiogope
Masela wataonaje
Wakiuliza usiongope
Wivu watapataje?
Sema nami wangu kipenzi
Twende sawa kila hatua
Tupo kwenye yetu enzi
Wasitushughulishe tusowajua
Sema nami tupo wawili
Dunia imetulia
Zima taa washa kandili
Mandhari iwe sawia
Tusemezane kiswahili
Kiingereza kimefulia
Vionjo vimenawiri
Hadi moyo wataka lia
Sema nami anza sasa
Kesho hatunayo ahadi
Sema jaza kurasa
Za kumbukumbu iwe yangu zawadi.

09/12/2017

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..