Sunday, February 7, 2016

Uzuri Wako
Uzuri wako ni zaidi ya ngozi nyororo
Zaidi ya macho ya kuvutia na mwendo wa maringo
Uzuri wako, haupimwi kwa mavazi wala kiasi cha sifa
ulizomiminiwa
Uzuri wako siyo mwanya wala vito vya thamani ulivyojaza shingoni
Wala siyo sauti ya kumtoa nyoka pangoni
Uzuri wako unatokea moyoni;
Vitendo vya ukarimu
Maneno ya busara
Heshima kwa wanadamu
Bila ya kujali fukara
Uzuri wako ni tabia zako,
Kujihifadhi na machafu kuyakimbia
Heshima kujijengea. madoa kutoitia
Uzuri wako ni zaidi ya lulu, UTHAMINI.

Usidanganyike na fedha ulizonazo mfukoni
Kamwe uzuri haununuliwi dukani
Usijitambe kwa barua lukuki ulizotumiwa
Na maneno mazuuri uliyotunukiwa
Wengi huitoa sukari wakijaribu kujinadi
Ukiwapa kidogo asali, huvunjika nayo ahadi
Uzuri ni zaidi ya sura
Asikuzuge mwanadamu
Uzuri wako siyo biashara
Kuuza ni haramu.
Uzuri kwa wote upo, wanawake na wanaume
Japo wengi husema, hasifiwi uzuri mwanamume
Lakini umeona wapi watu wakipenda vibaya?
Jaribu kuvaa viraka kama hukushikwa na haya
Kila utayemuita ataenda pitia mbali
Lazima safi kujiweka, ukitaka mpata mwali
Uzuri wako ni tabia, na mwenendo wa maisha
Uzuri wako hubakia, hata umri ukiisha
UTHAMINI.

(c) 2015

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..