Monday, August 8, 2016

NJOO NYUMBANI - EAVC 2016 PERFORMANCE PIECE

Umoja ni kupendana,
Umoja si kutengana,
Si kutendana,
Si kuchukiana,

Umoja ni kushikamana,
Umoja ni kushirikiana,
Ni kusaidiana,
Kuzijenga jamii,
Ni kusikilizana,
Maagano kuyatii,

Umoja ni kuhurumiana,
Umoja ni kuthaminiana,
Si kutukanana,
Si kuchuniana,

Umoja maana yake ni kuungana,  kushiriki kwa pamoja na kuelimishana,
Kuburudishana,
Kwenye mapungufu kuvumiliana,
Katu kutojali kutofautiana,
Kutothubutu kubaguana,
Kwa rangi, ama kabila, ama jinsia,
Kwa uwezo, ama maumbile, ama kwa mazoea,

Tumeumbwa na maulana kwa dhamira,
Kila mmoja kwa upekee wake amejaaliwa,
Kipawa cha kufanya mazito, makubwa na ya kusisimua,

Tumeelekezwa kuwa na subira,
Ili pamoja tuongozane kuipata dira,
Na Hilo ndilo Wazo la busara,
Kuwa na upendo wa dhati bega kwa bega,
Kuwa na umoja imara usiolega,
Kuwa kitu kimoja, kijiji, kata, wilaya, mkoa, nchi, bara na dunia,
Kuwa na hamasa, pale tunapoonana nafsi ziwe zenye kufurahia,

Nakuita Afrika, salamu nakutolea,
Nakuita dunia,  amani nakuombea,
Nakuita Afrika, moyoni upate tulia,
Nakuita dunia, mapenzi nikumiminie,
Njoo nikukumbatie.

(c) Zuhura Seng'enge
     ~ A. L August 2016

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..