Tuesday, March 15, 2016

Ndoto Kubwa

Nimejawa na ndoto za ushindi
Sipati usingizi
Mapenzi kwa familia hakuna wa kuyazidi
Ni jukumu kujituma
lazima kujitahidi
Kuzidi
Pambana na miba navyo visiki
Kuitafuta riziki
Iondoke yetu dhiki
Tupate faraja maisha yawe rahisi
Tupate kujenga jamii tunayoishi.

Nahangaika kuutafuta ushindi
Sitaki usingizi
Starehe ni gharama na kwetu hatuziwezi
Lazima kukazana ili niipate kazi
Inipatie malazi, chakula, mavazi
Isije niingia hulka ya ujambazi
Sitaki kuchetuka, nimeshaaga wazazi
Nimeshatoa ahadi
Rushwa kuiweka mbali na kukwepa ufisadi
Tamaa kuizuilia isijenigeuza hasadi.


Sitochoka kupigania ushindi
Ushindi nyumbani,
Ushindi wa upendo, usawa na amani
Kwa kila mwanadamu Afrika, na duniani
Isimwagwe hovyo damu
Kama ng'ombe machinjioni
Asiuzwe albino
Kama mbuzi mnadani
Sitaki
Kuona inapotea haki
Sheria isimame hata kwa wenye malaki
Tupo sawa watu wote hata tukiuza chaki
Maji, pipi, au mishikaki
Wanyonge nao watu sitopenda waonewe
Ndiyo mana nakazana mahitaji yao wapewe.


Maisha ni safari ya kusaka ushindi
Kufanya yaliyo mema
Kuzitafuta neema
Mungu anijaalie tabia iliyo njema
Ukweli siku zote niweze kuusema
Nikwepe shutuma za jamii na lawama
Niweze kuwa mshindi kwa baba na mama
Kwakweli Sitochoka!
Kwa nguvu nitasota!
Milima nitapanda, mabonde nitashuka
Majangwa nitapita, bahari nitavuka
Manyasi nitafyeka, visiki nitaruka
Pambano ntapigana, ushindi kuupata
Nia yangu kuu kuukamata ushindi
Peke yangu tuu nitasonga ikibidi
Niombeeni uzima nifike huko salama
Niokoe Tanzania kwenye wimbi la ujinga
Turudishe mshikamano kama enzi za ujima
Usawa kwa watu wote, walo bara na visiwa.
Ndoto yangu kubwa, Ndoto ya ushindi.

© Zuhura Seng'enge
~ A.L 2015

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..