Thursday, December 4, 2014

KWAKO NINATAMANIA.

Asubuhi inapofika maswali mengi hunijia
Wapi nitakwenda?
Nini nitakula?

Nikitangatanga kiguu na njia
Jua nalo likianza kusogea
Najiuliza wapi nitaanzia
Mawazo yanivaa na kutonesha vidonda

Maisha ya zamani nayatamania
Niliishi kwa amani sikuwahi fikiria
Kama shilingi mia itakua adimu,
Kama mkate ulooza nitalilia.

Usiku unapoingia hofu nyingi hunikaribia
Nani atanidhuru?
Wapi nitajilaza?

Ninaangaza huku na huko
Kutafuta hata boksi na mfuko
Tumbo likiunguruma kwa njaa
Ni siku ya tatu sasa, naanza kukata tamaa

Mvua ikininyeshea nimekaa pweke nikilia
Miaka sita nipo kitaa ndoto zangu zinanikimbia.

Asubuhi inafikia na huzuni yanivamia
Safari nyingine kiguu na njia
Kutafuta pakufikia

Nikigonga kwako nipokee
Hata shilingia mia nitolee
Nipate maji na andazi
Nisijechetuka nikafa jambazi.

Ewe unayetupa chakula
Huogopi hata Mungu?
Wengi tunakililia
Tulikombe hata jungu.

Usione udhia.

Zuhura Seng'enge.
20/11/2014.

(Please share, leave a comment)

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..