Monday, December 8, 2014

NITAMPIGANIA MWANAMKE.

Nimejawa huzuni, majonzi mengi moyoni
Dukuduku langu la siri ni kama kitanzi shingoni
Kifua changu kilichokua hifadhi ya mambo mengi, leo chakataa kutunza siri
Hakika huu ni udhalili
Macho yangu yaliojawa upendo na upole, leo yanachoma kama mishale
Machozi tele kwa tele
Sikujua ukimya wangu unaweza kua silaha
Ya kuongeza uovu na kupora amani na furaha
Sasa nimechoka kutazama wenzangu wakiumia
Nimechoka kuyafuta machozi yao wakilia
Nimechoka kuhudhuria misiba yao wakiangamia
Leo nasimama kupigania
Uhuru na utu wa mwanamke
Leo nasimama kutetea
Haki za msingi za mwanamke
Najitoa kumpigania mwanamke.

Nilijawa wasiwasi na hofu nyingi moyoni
Dukuduku langu la siri likanitia majutoni
Nilidhani nitavumilia na maisha yatasonga mbele
Ila kwa hakika nilipotea kwani mateso ndio yakazidi kujenga kilele
Sasa sitosubiri miujiza kutoka kwa Mungu
Nitashika risasi, jambia hata na rungu
Kupambana na adui alieleta hofu na kiza
Akamfanya mwanamke kibwagizo na kivutio cha kuingiza fedha
Leo nasimama  kupingana na dhana za mfumo dume
Nasimama kupigana na anaejiita baba, kaka, ndugu, jamaa na mume
Kisha akaweka majeraha ya wazi na siri kwenye maisha ya mwanamke
Nasimama kukemea ukatili kwa nguvu zangu zote
Nimechoka kuweka siri, kwani siri ya ugonjwa ni mauti
Sasa najitoa kumpigania mwanamke kwa yangu sauti.

I say No to violence today!

©Zuhura Seng'enge.
     08/12/2014.

(Please share, leave a comment)

No comments:

Post a Comment

Please share your thoughts and feelings..