Monday, December 29, 2014

SITAKI KUA MTUMWA.

" I'm your loyal servant! ''
Ulisema kwa ushupavu ukijiamini
Ukatia vionjo na ahadi nyingi
Kutupumbaza tusilione shombo
Kwenye kiti cha enzi ukila yamini
Kua utapiga vita rushwa na kutokomeza umasikini.
" I'm here to serve your needs! "
La hasha! Hukusimamia yako kauli
Ukaleta dharau na kiburi
Ukijitapa kwa nguvu na madaraka
Uliovikwa na unaowasulubisha
Nikatazama..
''A woman has no right to speak out! ''
Ikapigwa kampeni kwa tarumbeta
Wanawake tukakubali kukeketwa
Watoto wetu wakaachishwa shule mapema
Eti ni hasara kusomeshwa bora ya kuolewa
Tukakataliwa kujieleza na kuhitaji maendeleo
Tukafanywa kivutio cha biashara na vileo.
''A woman was born to serve a man! ''
Nyimbo tukaimbishwa tukumbuke hata usingizini
Tukafanya mazoea maisha yetu kutothamini
Tukakubali kunyanyaswa matope tukayaramba
Wakila zao kuku bata sisi tunakesha shamba,
Nikanyamaza..
''You are the only one for me! ''
Ukanipamba nikakubali kudanganyika
Kwa mapenzi ya kinafiki kila siku ukanizuga
Nikazama kwenye shimo la kenge na mamba
Majeraha nikayavaa nikazidi kuvuta kamba
Kwani kwako nilipenda
Na kwako nikachuma vidonda.
''You are more beautiful in a mini skirt! ''
Ati fasheni ndio alama ya uzuri wangu kwako
Nisipokaa uchi sio wa matawi kwako
Nisipojua kula bata siwezisimama pembeni yako
Nisipoweza kukatika siwezipata penzi lako
Nikakubali kunuka shombo
Nikidhani uzuri ni ule wa macho
Nikakufanya wangu mwandani
Kumbe kwako nimekua makombo
Nikakubali..
Nimeishi kwenye giza la utumwa wa nchi,
Utumwa wa nafsi, utumwa wa mwili
Ninajua mimi sio kiumbe kamili
Ila sitokubali kuendelea kuzama majini
Nimetazama ahadi zikivunjwa
Na wale niliowaamini kunitunza
Wakaapa kuongoza kwa haki
Kisha wakala mali zetu tukabaki kuuza mishikaki
Nimenyamaza wakati ninadhulumiwa
Elimu yangu kuonekana udhia
Maisha yangu kuwekwa kwenye mizani
Na wengine ndio wa kuyatia ama kutoa thamani
Nikakubali kuweka imani juu ya yule mtu
Anaependa kukosoa, asiethamini utu
Ambaye mapenzi kwaye ni mashindano
Anayefanya uzuri biashara ya mitandao.
Nimetazama!
Nikanyamaza!
Nikakubali!
Kuonewa na niliowaamini kwa moyo
Wakieneza gonjwa la woga katika jina la upendo
Sitaki tena kua mtumwa wa wanafiki na waongo
Sikubali kunyamaza kimya na kuwageuzia mgongo
Mkuki watanichoma nikiwa sina habari
Ila sasa nimewasoma sizami tena bahari.
©Zuhura Seng'enge.
  29/12/2014.
'' Slavery takes many forms. Beware of people who love you for your fame and your face, for they will always belittle your strengths.
He who loves you seeks not to possess you but to bring out the best in you.''
(Please share, leave a comment)

2 comments:

  1. Pongezi za dhati kwako mshairi kwa maana shairi ni.zuri sana! Na pongezi kwa kuupinga na kuukata utumwa!!

    ReplyDelete

Please share your thoughts and feelings..